WASICHANA nchini wameng’ara katika matokeo ya
mtihani wa darasa
la saba mwaka huu, baada ya kuongoza kwa asilimia 50.20 na kuwapita
wavulana waliopata asilimia 49.
80.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa, alitangaza
matokeo hayo jana wizarani kwake na kusema kuwa wanafunzi 560,706
wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za sekondari za
serikali.
Alisema, kati ya wanafunzi hao wasichana waliochaguliwa ni 281,460,
huku wavulana wakiwa 279,246, na hivyo kufanya idadi ya wanafunzi
waliochaguliwa kuongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na wanafunzi
515,187 waliochaguliwa awamu ya kwanza 2011.
Kawambwa alisema, mtihani huo uliofanyika Septemba 19 na 20, kwa mara
ya kwanza ulitumia teknolojia mpya ya ‘optical mark reader’ ambapo
mitihani ilisahihishwa kwa kutumia kompyuta.
Alisema utumiaji wa teknolojia hiyo mpya umeipunguzia serikali gharama
kwa kuwa mwaka jana walimu 4000 walitumia zaidi ya mwezi mmoja
kusahihisha mitihani hiyo nchi nzima, lakini kwa mwaka huu walimu 285 tu
ndio waliotumika kwa siku 15 kukamilisha usahihishaji huo.
“Matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi yanaonyesha kuwa
alama ya juu kabisa ilikuwa 234 kati ya 250 kwa wasichana na wavulana.
Matokeo hayo pia yanaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 3087 walipata
alama za daraja la A, wakati wanafunzi 40,683 walipata daraja la B.
“Jumla ya wanafunzi 222,103 walipata alama za daraja la C na 526,397
walipata alama za daraja la D. Waliobaki 73,264 walipata alama E,”
alisema Kawambwa.
Hata hivyo, waziri huyo katika maelezo yake, hakuweza kutaja mikoa
iliyofanya vema na ile iliyoshika nafasi ya mwisho. Kadhalika Waziri
Kawamba hakuweza kutoa nafasi ya kutosha kwa waandishi kuuliza maswali
kwa kile alichodai kuwa na haraka ya majukumu mengine ya kitaifa.
Akizungumzia udanganyifu katika mtihani alisema kuwa takwimu
zinaonyesha kuwa idadi ya watahiniwa waliofutiwa matokeo kutokana na
kujihusisha na vitendo vya udanganyifu katika mtihani huo imepungua.
Alisema waliofutiwa matokeo 2012 ni watahiniwa 293 tu ikilinganishwa
na watahiniwa 9736 waliofutiwa matokeo kwa undanganyifu mwaka jana.
“Kufuatia udanganyifu huo, serikali itawabaini wale wote waliohusika
katika udanganyifu huo na kuwachukulia hatua stahiki,” alisema.
kuhusu tatizo lililojitokeza mwaka jana la wanafunzi kutokujua kusoma
na kuandika, serikali imeanzisha mpango mpya wa kuwachuja wanafunzi hao
kwa kufanya mtihani mwingine kabla ya kuanza kidato cha kwanza.
Alisema, serikali inafanya hivyo ili kujihakikishia haitarudia kosa la
kuwapeleka wanafunzi wa aina hiyo sekondari, bali endapo watabainika
watafutiwa usajili na kupelekwa kwenye mfumo wa kujifunza kusoma na
kuandika.
Wanafunzi 894,839 wa shule za msingi walisajiliwa kufanya mtihani huo
wa kumaliza darasa la saba, wengine 29,012 sawa na asilimia 3.24
hawakufanya mtihani kutokana na sababu za utoro, vifo na ugonjwa.
|
|
0 comments:
Post a Comment