THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
press@ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Ndugu Irene
Charles Isaka kufuatia kifo cha ghafla cha Mwenyekiti wa Bodi ya
Mamlaka hiyo, Bwana Siraju Juma Kaboyonga.
Marehemu Kaboyonga ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini
kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), amefariki ghafla usiku wa
kuamkia leo tarehe 19 Desemba, 2012 katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili (MNH) alikokuwa amepelekwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo.
“Nimepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Bwana
Siraju Juma Kaboyonga ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya
Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) ambako
amefanya kazi kwa muda mfupi kabla mauti hayajamkuta”, amesema Rais
Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
“Nilimfahamu Marehemu Siraju Juma Kaboyonga, enzi za uhai wake, kama
Kiongozi na Mtumishi mwenye uwezo mkubwa aliouonyesha dhahiri alipokuwa
Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ambapo vipaji vyake alivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu
kuwatumikia kikamilifu Wananchi wa Jimbo la Tabora Mjini na kwa kweli
Umma wa Watanzania kwa ujumla”.
Rais Kikwete amesema ni uwezo wake huo mkubwa uliomwezesha kuteuliwa
kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya
Hifadhi ya Jamii (SSRA) ambako hakika mchango wake mkubwa unaonekana
dhahiri hivi sasa.
“Kufuatia msiba huu mkubwa, ninakutumia Salamu zangu za Rambirambi wewe
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi
ya Jamii (SSRA), Ndugu Irene Charles Isaka kwa kumpoteza Mwenyekiti wa
Bodi ya Mamlaka yako. Aidha kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu
zangu za Rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya Marehemu kwa
kupotelewa na Kiongozi, na kwa kweli Mhimili madhubuti wa Familia”.
Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee
na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu Siraju Juma Kaboyonga.
Amewahakikishia wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika kipindi hiki
kigumu cha maombolezo huku akiwataka wawe na moyo wa uvumilivu na
ujasiri katika kuomboleza msiba wa mpendwa wao, kwani yote ni mapenzi
yake Mola.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Desemba, 2012
0 comments:
Post a Comment