WAKATI msimu wa mavuno ukitarajia kuanza wilayani Njombe serikali wilayani humo imepiga marufuku ununuzi wa mazao kwa mtindo wa mshono maarufu kama lumbesha hasa zao la viazi mviringo.
Kwa mujibu wa barua iliyotumwa kwa chama cha wakulima na wasafirishaji kutoka ofisi ya mkuu wa wilaya ya Njombe na kusainiwa na mkuu wa wilaya hiyo bi. sara dumba inakitaka chama hicho kusitisha ununuzi wa zao la viazi mviringo kwa mtindo wa mshono lumbesa.
Aidha barua hiyo iliagiza mazao yote kuuzwa kwa mtindo wa mshono mfuto kwa kuzingatia sheria za vipimo cap. 340 revised edition ya mwaka 2002 na kwamba kwa yeyote atakaye kiuka agizo hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Katika barua hiyo imewataka watendaji wa kuanzia ngazi ya vijiji kuhakikisha wanasimamia zoezi hilo ili kuona agizo hilo linatekelezwa ipasavyo na kwamba atakayekiuka atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Agizo hilo la mkuu wa wilaya limekuja kufuatia malalamiko ya wakulima kuhusu suala la mshono lumbesa katika zao la viazi mviringo kuendelea kutekelezwa licha ya serikali kutoa maagizo mara kadhaa ya kusitisha ununuzi wa mazao kwa mtindo huo.
Hapo mwaka jana aliyekuwa naibu waziri wa viwanda na biashara Adam Malima alizitaka halmashauri za wilaya kushirikiana na viongozi wa mkoa ili kuhakikisha wanapiga marufuku na kuzuia ununuzi wa mazao kwa mtindo wa lumbesa hasa viazi mviringo.
0 comments:
Post a Comment