tg

Monday, December 31, 2012

JUMLA YALIYOTOKEA MWAKA MZIMA NJOMBE 2012

Jumla ya matukio 62 ya mauaji ya kukusudiwa yametokea katika mkoa wa Njombe kwa kipindi cha kuanzia Juni mosi hadi Disemba 29 mwaka 2012 huku vifo 33 vikiripotiwa. Hayo yamebainishwa na Ofisa Mnadhimu wa Jeshi la Polisi mkoa wa Njombe Focas Malengo, wakati akizungumza na waandishi wa habari  juu ya utendaji kazi
wa jeshi hilo katika kipindi cha miezi sita iliyopita tangu lilipoanza
kazi rasmi kimkoa Juni mosi mwaka huu baada ya Njombe kutangazwa rasmi kuwa mkoa.

Aidha Malengo alisema  watu 19 wameripotiwa kuuawa kwa kujinyonga,
huku matukio ya unyang’anyi wa kutumia ngunvu yakiwa 13, kukutwa na
bangi 26, kukamatwa na nyara za serikali mawili na uhamiaji haramu
mawili, ambapo jumla ya wahamiaji haramu 105 walikamatwa na kufikishwa
mahakamani.

Akizungumzia matukio ya ujambazi alisema jumla ya majambazi 20 wa
kutumia silaha za moto walikamatwa pamoja na silaha sita na kufikishwa
mahakamani.

“Bado tunayochangamoto kubwa ya kupambana na maovu hapa Njombe, maana
tangu tuanze kazi Juni mosi kumekutana na matukio ya ajabu yakiwemo
mauaji mengi, ili kukabiliana na matatizo haya lazima jamii
ishirikiane nasi ili tuweze kuangalia namna kukabiliana nayo,” alisema
Malengo.

Akizungumzia ajali za barabarani alisema jumla ajali 50 zimetokea
katika mkoa wa Njombe na kusababisha vifo vya watu 53 na majeruhi 48.

Alisema katika matukio ya ajali za barabarani pikipiki ndizo
zinaongoza kwani katika mwezi oktoba pekee jumla ya watu 18 walipoteza
maisha kutokana na ajali hizo.

Alisema kutokana na ajali hizo kwa sasa jeshi hilo limeanzisha program
maalum kwa ajili ya mafunzo ya madereva wa pikipiki mkoa mzima ili
kuweza kukabiliana na ongezeko la ajali hizo ambazo nyingi zinatokana
na uzembe wa madereva.

“Nawaomba madereva wafuate kanuni za usalama barabarani ili kuepuka
ajali hizi ambazo nyingi zinatokana na uzembe wa madereva,” alisema
Malengo.


Aliwataka madereva wa vyombo vya moto kufuata kanuni na sheria za
usalama barabarani na kuheshimu watumiaji wengine wa barabara ili
kuepuka ajali zisizo kuwa za lazima.

Malengo alisema makosa ya usalama barabarani bado ni changamoto katika
mkoa wa Njombe kwani tangu Juni mosi hadi Disemba 29 jumla ya makosa
6702 yameripotiwa na wahusika kutozwa faini, ambapo  jumla ya sh.
200.6 milioni zimepatikana na faini hizo.

0 comments:

Post a Comment