Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo leo wakati wa mahojiano maalum na mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com mjini Ludewa kuhusu mkakati wa wilaya wa katika kusimamia elimu ya sekondari kwa wale waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari .
Madaha alisema kuwa ili kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata haki yake ya msingi ya kuendelea na masomo ni vema kila mzazi kuhakikisha anatimiza wajibu wake kwa kumpeleka mtoto shule kama alivyochaguliwa badala ya kuwaruhusu watoto hao kwenda mijini kufanya kazi za ndani .
Hata hivyo alisema kuwa moja kati ya mkakati wa wilaya ya Ludewa ni kuhakikisha watoto wote waliofaulu kujiunga na elimu ya sekondari wanaanza masomo mapema zaidi na kuwa moja kati ya wajibu wa mzazi ni kumpeleka mtoto shule.
Pia alisema kuwa mbali ya kuwabana wazazi ambao watashindwa kusomesha watoto wao elimu ya sekondari pia serikali ya wilaya ya Ludewa itawachukulia hatua kali wale wote ambao watawakatisha masomo wanafunzi kwa kuwapa mimba pamoja na wazazi watakaotetea wanaume ambao wamewapa mimba watoto wa shule.
" Wapo baadhi ya wanaume ambao wamekuwa na tabia ya kuwarubuni watoto wa shule kwa mapenzi na kuishia kuwakatisha masomo kwa kuwapa mimba huku wazazi wakiwalinda watu hao ambao wanashindwa kuwatafuta akina asha Ngedere kwa maana ya wanawake wenye umri sawa na wao na badala yake wamekuwa wakikimbilia kufanya mapenzi na wanafunzi....nasema tutawabana wote na kuwafikisha polisi"
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa wilaya ya Ludewa imeendelea na mkakati wa kuwalinda watoto wa kike kwa kuendelea na ujenzi wa mabweni ili kuwanusuru watoto hao wa kike na vishawishi vya mapenzi kutoka kwa mafataki hao.
Alisema kuwa utaratibu huo wa kujenga mabweni utasaidia kuwafanya watoto wa kike kusoma bila kuwepo kwa vishawishi na kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakishawishika na kuingia katika vitendo vya ngono kutokana na kuishi nyumba za kupanga na kuishi mbali na shule.
Aidha alimpongeza mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe kwa jitihada zake za kuendelea kuwasaidia watoto yatima na wale wasiokuwa na uwezo wa kwenda sekondari pamoja na kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari.
Hivyo kuwataka madiwani na maofisa watendaji wa kata na vijiji kuendelea kuwajibika kwa kufuatilia maendeleo ya watoto hao .
Mbunge wa jimbo la Ludewa Bw. Filikunjombe alisema kuwa ofisi yake imekuwa na utaratibu wa kusomesha watoto 25 kwa kila kata kwa kata zote zaidi ya 23 za jimbo la Ludewa na kuwa moja kati ya sababu ya kufanya hivyo ni kuwasaidia watoto hao kupata haki yao ya elimu .
0 comments:
Post a Comment