tg

Thursday, March 13, 2014

MAHAKAMA YA MWANZO MAKETE MJINI YAMWACHIA HURU MTOTO WA MIAKA 17 ALIYEKUWA NA KESI YA WIZI



Watu watatu wamepandishwa kizimbani leo katika mahakama ya mwanzo Makete mjini kwa makosa tofauti akiwemo mtoto mwenye umri wa miaka 17 mkazi wa Lupila.

Akiieleza mahakama mwendesha mashitaka wa polisi PC Ally, mbele ya hakimu Happy Ngogo amesema mtuhumiwa huyo Hilary Massawe (17) mnamo Juni 26 mwaka jana aliiba mashine yenye thamani ya shilingi milioni 1.5 na sabini mali ya Daniel Okoka.

Hakimu Happy Ngogo amesema kutokana na sheria inayolinda haki ya mtoto mahakama hiyo inamkabidhi mtuhumiwa huyo chini ya ustawi wa jamii wilaya ya Makete ili kutenda haki ya mtoto huyo.

Hata hivyo washauri wa ustawi wa jamii Bi.Sechelela Dagaa na Bw. Leonce Panga waliamuru mahakama hiyo impe adhabu mtoto huyo.

Hata hivyo mahakama iliamua kumshauri mtoto huyo naye akakubaliana nao na kukiri kosa na kuahidi kurudisha mashine hiyo na mahakama hiyo kumsamehe kwa kutokumpatia adhabu yoyote, baada ya mtoto huyo kusema anauwezo wa kulipa gharama za mashine hiyo, hivyo ameachiwa huru

Katika tukio la pili Julidi Mahenge (21) mkazi wa Ujuni wilayani Makete amepandishwa kizimbani hapo leo kwa tuhuma za ubakaji.

Tukio hilo limetokea Machi 10 mwaka huu katika kijiji cha Nkenja kata ya Kitulo wilayani hapa ambapo inadaiwa mtuhumiwa alimbaka mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 (jina linahifadhiwa).

Hata hivyo mshitakiwa amekana shitaka linalomkabili na licha ya dhamana kuwa wazi, amerudishwa mahabusu kwa kukosa wadhamini hadi Machi 21 mwaka huu kesi hiyo itakapo tajwa tena.

Wakati huo huo Tumlaki Msigwa (21) mkazi wa Kitulo wilayani hapo amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za unyang`anyi wa kutumia nguvu.

Mwendesha mashitaka wa polisi PC Ally mbele ya hakimu Happy Ngogo ameeleza kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hiloMachi 10 mwaka huu ambapo alimkaba na kufanikiwa kumpora Pelesi Mwaigaga fedha taslimu shilingi 700,000/=

Hata hivyo mshitakiwa amekana shitaka hilo na amerejeshwa rumande kwa kukosa wadhamini hadi Machi 21 mwaka huu kesi yake itakapotajwa tena.

Mwendesha mashitaka wa polisi PC Ally ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Machi 10 mwaka huu saa nne usiku
 
Na Henrick Idawa

0 comments:

Post a Comment