Balozi
wa Tanzania Nchini Ethiopia, Joram Biswaro, amewataka Wachezaji wa
Taifa Stars kuhakikisha wanaipeleka Timu hiyo kwenye Fainali za Kombe la
Dunia zitakazofanyika mwakani Nchini Brazil.
PATA HABARI KAMILI:
Release No. 093
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mei 30, 2013
BALOZI BISWARO AWAPA CHANGAMOTO STARS
Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia,
Joram Biswaro amewataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanaipeleka
timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani
nchini Brazil.
Ametoa changamoto hiyo wakati
alipotembelea mazoezi ya timu hiyo jana (Mei 29 mwaka huu). Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga kambi nchini
Ethiopia na inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Addis Ababa.
“Watanzania tunafurahi kutokana na uwezo
mnaouonyesha, hasa baada ya kuifunga Morocco mabao 3-1. Kama mliwafunga
nyumbani hata kwao mnaweza kuwafunga. Tunataka kuwaona Maracana
(Brazil) mwakani, mimi tayari ninayo tiketi mtanikuta kule,” amesema
Balozi Biswaro ambaye enzi zake aliwahi kuichezea timu ya Yanga.
Taifa Stars ambayo iko Addis Ababa tangu
Jumatatu (Mei 27 mwaka huu) imeweka kambi katika hoteli ya Hilton
ambapo Jumapili (Juni 2 mwaka huu) itacheza mechi ya kirafiki na Sudan
(Nile Crocodile) kwenye Uwanja wa Addis Ababa.
Balozi Biswaro ameikaribisha Taifa Stars
ubalozini Addis Ababa mara baada ya mechi dhidi ya Sudan ambapo
itakutana na baadhi ya Watanzania wanaoishi Ethiopia kabla ya kuondoka
alfajiri kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri.
Kocha Kim Poulsen amesema kikosi chake
kinaendelea na mazoezi vizuri na kitaimarika zaidi baada ya wachezaji
Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kujiunga nacho Juni 3 mwaka huu
jijini Marrakech kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8
mwaka huu.
Wachezaji walioko katika kikosi cha
Stars jijini Addis Ababa ni Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally,
Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub
Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri
Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas,
Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Addis Ababa
0 comments:
Post a Comment