Jeshi
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeshitushwa na kusikitishwa kuona
taarifa ya mtu aliyejitambulisha kuwa askari wa JWTZ wa Kambi ya
Monduli, Arusha, iliyochapishwa katika gazeti la Mwananchi la Desemba
24, 2012 akiwa amevaa sare za JWTZ.
Baada
ya kuona habari hii JWTZ linafanya uchunguzi wa kina ili kutambua kama
mtu huyo ni askari wa kweli au la.
Kimsingi, JWTZ linafanya uchunguzi
wa kumtambua mtu huyo kama kweli ni askari wake kwa sababu zifuatazo;
kwanza Jina la mtu huyo halijaandikwa, pili kikosi halisi cha mtu huyo
hakijaandikwa kwani eneo la Monduli lina vikosi vingi na hakuna kikosi
kiitwacho Monduli.
Lakini
pia inatia shaka kuwa mavazi yale siyo yale yanayotumika kwa wanajeshi
wa JWTZ hivi sasa, kuna tofauti kati ya jampa (jacket) na suruali kama
ilivyooneshwa katika picha hiyo.
Aidha,
jampa la sare hiyo pia lina tofauti katika sehemu za mikono, jambo
ambalo linatia shaka kama ni sare halisi ya JWTZ. Ilikuwa rahisi
kumtambua mtu huyo kwa kuangalia uso, lakini mtu huyo anayedaiwa kuwa ni
askari alifunika paji la uso ili asitambulike.
Pamoja
na hali hiyo ilivyojitokeza, JWTZ linashughulika kumtambua mtu huyo kwa
kutumia mbinu mbalimbali.
JWTZ litakapobaini ukweli huo, hatua za
kinidhamu zitachukuliwa kutokana na Kanuni za Majeshi ya Ulinzi kwani,
Sheria nambari nne (4) ya mabadiliko ya nane (8) katika Katiba ya Nchi
ya mwaka 1992 ibara ya 147(3), mwanajeshi yeyote hatakiwi kujihusisha
katika masuala ya kisiasa.
Kama
ilivyoelezwa hapo juu, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
limesikitishwa kuchapishwa kwa picha hiyo kwani hakuna tija wala faida
kwa wananchi wa Tanzania zaidi ya kuwatia hofu kuwa Vyombo vya Ulinzi
navyo vinashabikia mambo ya siasa, wakati Katiba ya nchi imekataza jambo
hilo.
JWTZ linawaomba wananchi waliangalie jambo hili kwa makini, kwa usalama wa nchi yetu.
Imetolewana Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
SLP 9203,
Simu: 0764 742161
Email:ulinzimagazine@yahoo.co. uk
0 comments:
Post a Comment